Binti anusurika kifo kwa kula dawa ya panya

MSICHANA anayekisiwa kuwa na umri wa miaka (23), mkaazi wa Kinduni Mkoa wa Kaskazini Unguja, amenusurika kufa baada ya kunywa sumu ya panya kutokana na kukataliwa na mpenzi wake.

Msichana huyo alikataliwa na mpenzi wake  baada ya kuhitilafiana walipokuwa wakisherehekea sikukuu ya eid iliyomalizika hivi karibuni.

Taarifa zilizopatikana kutoka kwa watu wa karibu wa msichana huyo, alitenda kosa hilo usiku Juni 7 mwaka huu mara tu baada ya kurejea akitokea sikukuuni na mpenzi wake ambapo inadaiwa kuwa wana uhusiano wa siku nyingi.

Baada ya kula dawa hiyo na afya yake kuanza kutetereka, alikimbizwa hospitali ya Kivunge kwa ajili ya kupatiwa matibabu ambapo alilazwa kwa muda wa siku tatu na ameruhusiwa kutoka hospitalini hapo Juni 11.

Hata hivyo, kijana huyo atatakiwa kujibu tuhuma zake baada ya kupata nafuu na yupo nyumbani kwao Kinduni akiendelea kuimarisha afya yake.

Daktari kutoka hospitali ya kivunge ambaye hakutaka kutajwa jina lake Gazetini kwa masharti ya ripoti hiyo kupatikana kwa jeshi la Polisi Mkoa wa Kaskazini Unguja, kuwa ndio wanaotoa taarifa za matukio yote yanayohusiana na mkoa huo alithibitisha kumpokea binti huyo na kumfanyia uchunguzi na hali yake inaendelea vizuri.

Gazeti hili lilifanya mahojiano kwa njia ya simu na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kaskazini Unguja, Kamishna Msaidizi wa Polisi Haji Abdalla Haji kujua undani wa taarifa hizo alisema hakuna taarifa hizo kituoni na hajui taarifa hizo zimeripotiwa kituo gani.

CHANZO: ZANZIBAR LEO

error: Content is protected !!