Biashara ya viatu yampandisha kizimbani ‘Machinga’

MAHAKAMA ya mwanzo Malindi, imemtia hatiani Issa Ali Hassan (28) kwa kosa la kufanya biashara katika maeneo ya wazi.

Mshitakiwa huyo ambae ni mkaazi wa Bububu wilaya ya Magharibi ‘A’ mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, alikutikana akifanya biashara katika maeneo hayo jambo ambalo ni kinyume na kifungu cha 17 na 53 ya adhabu sheria ndogo ndogo za Baraza la Manispaa Mjini za mwaka 2004.

Mshitakiwa alikutikana akitenda kosa hilo, Disemba 3 mwaka huu majira ya saa 8:00 za mchana maeneo ya benki ya Bacley, alipatikana na kosa la kufanya biashara ya kuuza viatu, eneo ambalo haliruhusiwi kisheria.

Akisomewa shitaka lake na Mwendesha Mashitaka wa mahakama hiyo, Suleiman Khalfan Masoud, mbele ya Hakimu Nassem Fakih Mfaume, alikubali kosa lake na kuiomba mahakama imsamehe kwani hatorejea tena kosa hilo.

Kwa upande wa mashitaka ulidai kuwa hauna kumbukumbu ya makosa ya zamani kwa mshitakiwa huyo, hivyo adhabu itolewe kwa mujibu wa sheria inavyoelekeza.

Mahakama baada ya kujiridhisha na maelezo hayo, mshitakiwa alitiwa hatiani kwa kutoleshwa faini ya shilingi 50,000 au Chuo cha Mafunzo kwa muda wa mwezi mmoja, alipe fidia ya shilingi 50,000 kwa Manispaa Mjini.

Hadi Mwandishi wa habari hizi anaondoka mahakamani hapo mshtakiwa alifanikiwa kulipa faini na fidia ili kujinusuru kwenda jela kwa muda wa mwezi mmoja.

CHANZO: ZANZIBAR LEO

error: Content is protected !!