Balozi Seif awapongeza vijana kwa ubunifu

MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi (kushoto), akikabidhiwa zawadi kutoka kwa mmoja wa kiongozi wa kampuni ya kurahisisha huduma za Usafiri salama na uhakika (TANTAX), Salma Salum Othman. Uongozi wa kampuni hiyo jana ulikwenda ofisini kwa Makamu wa Pili wa Rais na kufanya mazungumzo naye. (PICHA NA OMPR).

MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, amewapongeza vijana wazawa walioamua kubuni mfumo mpya wa usafiri wa taxi ujulikanao kama Tan Tax.

Alisema ubunifu wao ambao unaungwa mkono na serikali, utasaidia kutoa fursa za ajira ambazo kwa sasa zina changamoto hasa kwa vijana wanaomaliza masomo yao.

Alitoa pongezi hizo ofisini kwake Vuga mjini Zanzibar wakati akizungumza na timu ya viongozi wa mfumo huo iliyofika kujitambulisha wakijiandaa kuuzindua mfumo huo.

Alisema serikali muda wote inahimiza umuhimu wa ubunifu katika nyanja mbali mbali ndani ya jamii ambazo hatma yake huleta faraja ya upatikanaji wa maendeleo na kupunguza au kuondosha kabisa changamoto zinazoizunguka jamii.

Alisema wakati umefika kwa jamii hasa vijana kuondokana na mawazo ya kufikiria ajira kutoka serikalini.

Mapema Mkurugenzi Mkuu wa mfumo huo, Salma Salum Othman, alisema lengo la kubuniwa mfumo huo ni kupata suluhu la tatizo la usafiri wa taxi.

Alisema dereva au abiria atakayeridhika kupata huduma kupitia mfumo atatakiwa kujiunga kwenye mfumo husika kupitia simu yake ya mkononi.

Naye Mhandisi Mkuu wa mfumo huo,Haji Masoud Abass, alimueleza Balozi Seif kwamba dereva ambaye atakuwa mwanachama atasajili bima, ruhusa ya barabara pamoja na  leseni yake ili kuwekwa katika mfumo huo.

Alisema abiria atakayehitaji usafiri atatumia mfumo huo kupitia simu yake ya mkononi itakayomuwezesha kupata huduma kwa haraka.

Kwa upande wake Naibu Mkurugenzi wa mfumo huo, Abass Salum alisema kutakuwa na ukurasa maalum katika njia ya mtandao wa mawasiliano katika kutoa taaluma kwa umma juu ya mfumo huo.

Alisema uzinduzi wa mfumo huo unatarajiwa kufanywa katika ukumbi wa Taasisi ya Kiswahili na Lugha za Kigeni Zanzibar, Julai 7.

error: Content is protected !!