Baada ya tetesi za kufutwa kazi kufuatia kufeli mazungumzo, dada wa Kim Jong-un aonekana Pyongyang

Baada ya kuenea habari za kupigwa kalamu nyekundu na Kim Jong-un, Kiongozi Mkuu wa Korea Kaskazini, hatimaye Kim Yo-jong, dada wa kiongozi huyo ameonekana kando na kaka yake katika moja ya sherehe mjini Pyongyang na hivyo kuhitimisha tetesi hizo zilizoanza kuenezwa siku 50 zilizopita.

Wiki iliyopita, gazeti la Chosun Ilbo la nchini Korea Kusini liliandika kwamba, kufuatia kuvunjika mazungumzo ya nyuklia kati ya Kim Jong-un na Rais Donald Trump wa Marekani mwezi Februari mwaka huu huko mjini Hanoi, Vietnam, Jong-un alitoa amri ya kumpunguzia cheo dada yake ambaye alihusika katika mazungumzo hayo. 

Katika uwanja huo Jumanne iliyopita vyombo vya habari vimetangaza kwamba, Kim Yo-jong, dada kijana wa Kiongozi wa Korea Kaskazini alionekana kwa mara ya mwisho katika kikao cha Bunge la nchi hiyo mwezi Aprili mwaka huu. Inafaa kuashiria kuwa Kim Yo-jong ni kati ya viongozi wa ngazi ya juu wa chama tawala nchini Korea Kaskazini na inaelezwa kwamba, ni mtu wa karibu sana na mwenye kuaminiwa na Kim Jong-un.

Kim Yo-jong alishirikiana na kaka yake katika mazungumzo kati ya Korea Kaskazini na Rais Donald Trump wa Marekani na Rais Moon Jae-in wa Korea Kusini. Kabla ya hapo pia baadhi ya vyombo vya habari vilitangaza kwamba, mjumbe maalumu wa nyuklia wa serikali ya Pyongyang kwa ajili ya mazungumzo na Marekani pamoja na maafisa wa ngazi ya juu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya nchi hiyo walinyongwa kwa tuhuma za kufanya ujasusi kwa maslahi ya Marekani. Habari hiyo ilikadhibishwa baadaye na serikali ya Korea Kaskazini.

error: Content is protected !!