Aliyekuwa msanii wa maigizo na vichekesho Juma Haji, ‘Halikuniki’, aliyefariki usiku wa kuamkia leo

UONGOZI wa Chuo cha Mafunzo Zanzibar umeungana na familia ya aliyekuwa msanii wa maigizo na vichekesho Juma Haji, ‘Halikuniki’, aliyefariki usiku wa kuamkia leo.

Akizungumza na gazeti la Zanzibar Leo, Afisa Michezo na Utamaduni wa jeshi hilo Khamis Machenga, amesema kuwa kifo chake kimeacha pengo kubwa na si kwa jeshi lao tu bali kwa tasnia nzima ya Sanaa ya Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.

Alisema kuwa marehemu pamoja na kuwa hakuwa mfanyakazi wao tena lakini bado walikuwa wanashirikiana nae katika masuala ya Sanaa.

” Kifo chake tumekipokea kwa masikitiko alikuwa ni msanii ambae tulishirikiana nae na alileta mchango mkubwa katika jeshi letu”, alisema.

Alieleza kuwa pamoja na kuwa kifo kimeumbwa lakini watamkumbuka kwa mchango wake na wanaungana na familia na wadau wa tasnia ya Sanaa katika kipindi chote cha maombolezo.

“Halikuniki yeye hakua mfanyakazi wetu tena lakini alikuwa bado anashirikiana na wasanii wetu hapa idarani kwetu, katika mambo mbali mbali ya kisanaa hata katika baadhi ya matangazo alikuwa akishirikiana na wafanyakazi wetu,” alisema.

Marehemu Halikuniki aliuguwa kwa muda mfupi na kufariki usiku wa kuamkia leo na kuzikwa kijijini kwao Donge Mkoa wa Kaskazini Unguja.

CHANZO: ZANZIBAR LEO

error: Content is protected !!