Abdulwakati: Nyota asiyesahaulika katika soka, tenisi Zanzibar

ZANZIBAR ni moja ya nchi ambayo imejaaliwa kuwa na vipaji vya aina mbali mbali, vikiwemo vya soka ambavyo kwa kiasi fulani vilitamba katika michezo hapa nchini.

Miongoni mwa watu waliotamba katika mchezo wa soka na mpira wa meza ni Abdullah Juma Aley maarufu Abdulwakati ambae alitikisa ndani ya Zanzibar na nje ya nchi.

Kama utataja majina ya watu waliowahi kutamba visiwani humu katika mchezo wa mpira wa meza na soka bila ya kumtaja Abdulwakati itakuwa hukumaliza idadi yao.

Abdullah Juma Aley ndio jina lake alilopewa na wazazi wake,lakini, hata hivyo jina hilo linafahamika kwa watu waliokuwa sio wengi kwani ukipita katika mitaa mingi ya visiwani humu ikiwemo Kikwajuni na kumtaja jina la Abdullah hutompata mpaka utaje Abdulwakati.

Jina hilo ndio limekuwa maarufu kwa kipindi chote alichocheza michezo hiyo na kuwika ndani ya Zanzibar,Tanzania,Afrika Mashariki na hata Arabuni.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, alisema, jina la Abdulwakati halitokani na kitu chochote isipokuwa ni mchezo wa soka ambao ulimpatia umaarufu mwaka 1980 na kuendelea.
Alisema kwamba jina la Abdulwakati alilipata wakati alipokuwa mdogo akichezea timu ya Hero Boys ambapo alisema alibatizwa na mwalimu wake wa soka, Abubakar Soni.

“Katika timu yetu kulikuwa na wachezaji watatu na wote walikuwa na majina ya Abdul, hivyo kututafautisha akaamua mimi kuniita Abdulwakati kwa vile nilikuwa nachezea nafasi ya mshambuliaji wa kati,”alisema.

Mchezaji huyo mkongwe ambae kwa kawaida ni mcheshi,alisema wachezaji wenzake walibatizwa majina mengine kama vile Abdul Kikono na Abdul Kifupi.

Katika maisha yake ya soka,alianza kung’ara mapema utotoni mpaka kupewa mikoba ya unahodha kwenye timu ya skuli visiwani Zanzibar.

Aliendelea kucheza timu ya watoto kabla ya kujiunga na klabu ya Everton iliyokuwa na maskani yake katika mtaa wa Kikwajuni mjini Unguja mnamo mwaka 1970.

Kutokana na uwezo wake mkubwa wa kusakata kabumbu, Abdulwakati alichukuliwa na timu iliyokuwa ikimilikiwa na kituo cha kulelea watoto cha Forodhani iliyokuwa ikijulikana

kwa jina la Karume Boys na kutembea nayo katika mikoa mbali mbali ya Tanzania.
Timu hiyo ambayo ilikuwa chini ya uangalizi wa rais wa Kwanza wa Zanzibar Marehem Mzee

Abeid Amani Karume ambapo ilikuja kugawanyika mara baada ya kifo cha kiongozi huyo mwaka 1972.

Alisema, akiwa katika kikosi hicho cha Karume Boys alikutana na wachezaji wengi akiwemo Sihaba Saadat, Omar Willium na wengine wengi.

Baada ya kusambaratika kwa Karume Boys,Abdulwakati alijiunga na Small Simba baada ya kushawishiwa kufanya hivyo na kocha wa zamani wa kikosi hicho,Masoud Salum ‘Masoud Kocha’.

Kutokana na ari,jitihada na moyo wake wa kusakata kabumbu wakati anapokuwa uwanjani,veterani huyo alichaguliwa kujiunga na timu ya taifa ya vijana ya Zanzibar mwaka huo 1972.

Akiwa na Small Simba, Abdulwakati alikuwa kivutio kikubwa sawa na wachezaji wote wa timu hiyo iliyojipatia umaarufu mkubwa baada ya kupanda daraja,ambapo ilianza kwa moto mkubwa na kutikisa vigogo vya soka nchini.

Alisema, timu yao ilikuwa imesheheni vipaji na kuwa gumzo la mji na kuanza kujitwalia ubingwa wa soka visiwani mwaka huo waliopanda ngazi 1983.

Chini ya nyota mahiri, Small Simba iliweza kutamba vilivyo katika miaka 1985 hadi 1987.
“Kuanzia mwaka 1983 hapo moto wetu ulikuwa hauzimiki na mashabiki wetu wakapata wimbo wa ‘Moto Small’ ambapo kila tulipokuwa tunashuka dimbani au watu walipokuwa wakizungumzia timu yetu waliimba”, alisema, mwanandinga huyo.
Jambo ambalo nyota huyo alisema, atabakia akilikumbuka maishani kwake ni tukio la mwaka 1987 kwa Small Simba kupokonywa ubingwa na Miembeni ambao walikwenda mahakamani.

Alisema anafahamu kwanini walishindwa kesi hiyo na kila mmoja alijua kutokana na hakimu wa kesi hiyo alikuwa Miembeni damu,hivyo alisema haki haikutendeka.

Abdulwakati alisema kwamba sababu za kwenda mahakamani wenzao na kupokonywa ubingwa kumetokana na wenzao wa Miembeni kudai kwamba walimchezesha mchezaji Shaban Mussa ambae hakuwa halali,licha ya Chama cha Soka Tanzania (FAT), kuthibitisha mahakamani kuwa mchezaji huru.

Umahiri wake katika soka uliwashawishi wahusika wa juu kumuita kwenye timu kubwa mwaka 1984 na kushiriki katika michuano ya Chalenji iliyofanyika mjini Mombasa nchini Kenya.

Milango ya heri ikamfungukia siku chache baada ya kurudi kutoka Mombasa,ambapo mashushu wa Oman walikuwepo kusaka wachezaji wa kuwapeleka kwao.

Alisema, mwaka 1984 Abdulwakati alitua rasmi nchini Oman na kuanza kuwasuuza roho Waarabu kwa ufundi wake wa kumiliki mpira na kupachika mabao.

Alisema mechi yake ya kwanza ilikuwa kati ya Oman na Qatar katika michuano ya ubingwa wa nchi za Ghuba akicheza kwa dakika 20 tu.

Aidha, katika mechi ya kihistoria iliyochezwa Riyadh, Saudi Arabia ikiwa ni michuano ya Gulf ushindi wa kwanza kwa Oman ulipatikana baada ya kurudi kambi nchini Brasil ambapo

Abdulwakati alifanikiwa kuipatia timu yake goli moja na timu yake kuibuka na ushindi wa magoli 2-1.
Kutokana na kipigo hicho Qatar ilimkatika rufaa Abdulwakati kwa madai kwamba ni mgeni,lakini rufaa hiyo ilishindwa kwani nao pia walikuwa na wachezaji kutoka Somalia wawili.

Hata hivyo mchezaji huyo alikuwa halali kuchezea timu hiyo ya Oman kutokana na kufanyiwa taratibu zote za uraia.
Baada ya hapo akawa anapangwa mechi zote kwa dakika 90 na kuwashangaza matajiri wake kwa kipaji alichokuwa nacho.

Anakumbuka matokeo mazuri ni yale ya sare1-1 walipocheza na U.A.E ambao ni wapinzani wakubwa wa Oman sawa na timu za Kenya na Uganda.
Anafahamisha kwamba kila mwaka Oman ilikuwa ikishika mkia katika mashindano ya ‘Gulf Cup’ lakini katika mashindano hayo walishika nafasi ya nne kati ya nchi sita.

Pamoja na mafanikio makubwa aliyoyapata katika nchi ya Oman,mchezaji huyo anakumbuka kadhia iliyowakasirisha wachezaji baada ya kutwaa ubingwa wa Ghuba ambapo chama cha soka na Wizara husika kushindwa kutimiza ahadi zao kwamba wangewapa zawadi nono.

Akiwa na timu hiyo,mwanasoka huyo veterani alifanikiwa kwenda katika nchi zote za ghuba kushiriki michuano hiyo inayochezwa kwa zamu.

Katika kumbukumbu yake alifahamisha kuwa wakati wakijiandaa na mashindano ya Bahrain walipiga kambi nchini Ufaransa na akabahatika kufundishwa na kocha Omar Boras raia wa Uruguay mwaka 1988 hadi 1990, ambae alikuwa kocha wa nchi yake katika mashindano ya Kombe la Dunia yaliofanyika Mexico mwaka 1986.

Alisema, baada ya kumaliza waliyotumwa kwa Oman kuwa mabingwa wa Ghuba zilijitokeza baadhi ya timu kumtaka na hatimae alijiunga na klabu maarufu ya Fanja ya Oman.
Wakati huo alisema alikuwa ni Mtanzania wa kwanza kujiunga na Fanja mwaka 1985,kabla ya kina Ahmed Amasha,Talib Hilal,Zahor Salim na Hilal Hemed.

Akiwa na timu hiyo aliiwezesha kutwaa ubingwa wa Oman mara nyingi sambamba na kombe la Sultan Qaboos kuanzia mwaka 1985 hadi 1992.
Aidha, alisema, mwaka 1987 alirejea Zanzibar kwa ajili ya mapumziko na kwenda na timu ya taifa nchini Ethiopia kwenye Chalenji ambapo walitoka sare na Kenya huku Tanzania

Bara wakiifunga magoli 2-0 na kutoka sare na Ethiopia katika mechi ambayo mlinda mlango alikuwa Ali Bushiri ambae aliokoa kwa penalti.

Hata hivyo kikosi hicho kilichokuwa kikinolewa na makocha Gulam Abdallah na marehemu Mzee Kheri kilitolewa na Zimbabwe katika hatua ya nusu fainali.
kitendo cha mwamuzi kuwabeba Wazimbabwe kilichangia kufungwa kwani walipokua nyuma kwa mabao 2-1, Inocent Haule alisawazisha lakini likakataliwa.

Abdulwakati ambae tangu akiwa kinda,alikuwa na lengo la kuchezea soka la kulipwa, alisema, aliwahi kushawishiwa na viongozi wa Simba wakati huo akiwa na timu ya Taifa Stars lakini aligoma kwa vile hakutaka kuihama Small Simba.

error: Content is protected !!