6.2b/-kung’arisha miji Pemba

JUMLA ya shilingi bilioni 6.2 zinatarajiwa kutumika katika kazi za uwekaji wa taa za barabarani, katika mji wa Mkoani, Chake Chake na Wete kupitia mradi wa ZUSP awamu ya pili.

Kazi hiyo ambayo itafanywa na kampuni ya Salim Construction ya Tanzania, tayari kazi ya utengenezaji wa vifaa imeanza, huku wilaya ya Mkoani taa hizo zikianzia kufungwa Changaweni hadi Jaalini eneo lenye urefu wa kilomita tano.

Katika wilaya ya Chake Chake mradi huo utaanza  Chanjaani  hadi Machomanne na Wete utaanzia Limbani, Kizimbani, Bandarini na Bopwe eneo lenye urefu kilomita saba.

Akizungumza katika majumuisho na watendaji wa mabaraza ya miji Pemba, Waziri wa Fedha na Mipango, Balozi Mohammed Ramia, aliwataka wananchi ambao bado hawajanufaika na miradi ya ZUSP kuwa na subira.

“Kwa wale ambao wamenufaika na miradi ya ZUSP awamu ya kwanza, kazi kubwa kwao ni kuhakikisha wanaitunza na kuithamini miradi hiyo kwa kuhakikisha wanaiwekea mazingira mazuri ya usafi,”alisema.

Alisema miradi ya mitaro katika awamu ya kwanza imewasaidia wananchi wa Unguja na Pemba, kwani maeneo ambayo yalikuwa yakituama maji sasa yako salama.

Aidha aliwataka watendaji kuhakikisha wanakuwa makini wakati wa utekelezaji wa mradi huo.

“Mradi huu wa ZUSP unaisha Juni 2020, tutahakikisha tunatelekeza kila kilichoainishwa na baraza la mji au halmashauri,” alisema.

Mkuu wa Wilaya ya Chake Chake, Rashid Hadid Rashid, aliipongeza serikali chini ya uongozi wa Dk. Shein, kwa kulipatia baraza la mji Chake Chake miradi mitatu ikiwemo ujenzi wa ofisi ya baraza hilo, chinjio la ng’ombe Tingatinga na ujenzi wa vidaraja.

Aidha alisema tayari mapendekezo yao wameyawasilisha ZUSP ili kuhakikisha barabara ya Ndugukitu Mkoroshoni inawekewa lami.

Aidha aliahidi kuhakikisha wanashirikiana na mkandarasi wa kazi ya uwekaji wa taa za barabarani, ili kuhakikisha mradi huo unamalizika kwa wakati.

Hata hivyo, alimuomba Waziri wa Fedha kuangalia kwa kina kazi ya uwekaji wa taa kufika hadi maeneo ya Gombani na Wawi.

Mkurugenzi wa Baraza la Mji Chake Chake, Salama Abuu Hamad, alisema kupitia mradi wa ZUSP awamu ya pili, zaidi wameangalia barabara za ndani kwani huwa hazipitiki wakati wa mvua.

Akizungumzia taa za barabarani, Mkurugenzi huyo aliahidi kuhakikisha mradi huo unasimamiwa vyema na unakamilika kwa wakati.

Mratibu wa mradi wa ZUSP Zanzibar, Makame Ali Makame, alisema tayari miradi mingi ya ZUSP imekabidhiwa, hivyo matengenezo madogo yatakayotokea yanapaswa kufanywa na taasisi husika.

CHANZO: ZANZIBAR LEO

error: Content is protected !!