Sunday, July 3
Shadow

Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi – Pemba yaunga mkono juhudi zinazofanywa na taasisi ya Shaibu Foundation

Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi – Pemba imeiunga mkono taasisi ya Shaibu Foundation kwa kuiruhusu taasisi hiyo kutumia vituo vyake vya TEHAMA-JAMII kwa lengo la kusaidia kufanikisha mradi wake ujulikanao kama  “e-Learning for Primary & Secondary Schools’ Project – Phase Two”

 

Akikabidhi barua ya udhibitisho wa kukubali taasisi hiyo kutumia vituo hivyo katika ufundishaji Ahmed B. Said kwa niaba ya Ofisa mdhamini amesema wizara haina pingamizi juu ya matumizi ya vituo hivyo vya Tehama kwa kuwafundisha walimu kwani itasaidia kukuza taaluma kwa walimu hao na kuwa na weledi zaidi katika ufundishaji. Vituo hivyo vitatumika kwa skuli zilizo karibu na ambao hawana vifaa vya Tehama au Chumba cha Computer kwenye skuli husika.

 

Akieleza Lengo kuu hasa la mafunzo hayo Rais wa Shaibu Foundation Mustafa Moyo amesema ni kuwajengea uwezo na kuwaunganisha walimu na fursa zinazotokana na TEHAMA kama vile kufundisha, kujifunza kwa kupitia elimu masafa, kutumia vifaa vya Tehama kufundishia ili kuongeza ubunifu darasani na kuwafanya wanafunzi kupenda mazingira ya kujifunzia.

 

Amevitaja vituo vitakavyotumika ni Kituo cha Tehama Micheweni, Machomanne na Kituo cha Mkoani.

 

Ndugu Ahmed B. Said (kushoto) kutoka Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi akimkabidhi barua ya uthibitisho wa ruhusa ya kutumia vituo vya Tehama Jamii Ndugu Mustafa Moyo kutoka Shaibu Foundation.

 

Mradi huu ulioanzishwa mnamo mwaka 2018 kwa awamu ya kwanza, ambapo baadhi ya walimu skuli ya Madungu Msingi walinufaika na mradi huo kwa awamu ya kwanza.

 

Awamu ya Pili ulizinduliwa rasmi tarehe 26/06/2021, ambapo zaidi ya skuli 13 kisiwani Pemba zitanufaika.

 

Mafunzo hayo kwa walimu yatawaongezea ujuzi mpya ambao utawafanya kuwa wabunifu zaidi na kuweza kuzitumia fursa zilizopo na  zinazotokana na Tehama.