Waziri: Wanahabari msivae magwanda ya kisiasa

Na Salum Vuai, WHUMK

VITUO vya habari vinavyoendelea kuanzishwa visiwani Zanzibar, vimeshauriwa kutoegemea upande wowote kisiasa vinapotoa habari zao hasa katika vipindi vya uchaguzi.

Waziri wa Habari, Utalii na Mambo ya Kale Mahmoud Thabit Kombo, amesema serikali inavipa leseni vyombo hivyo ili visaidie kuielimisha jamii juu ya mambo mbalimbali ya maendeleo na umuhimu wa kuendeleza amani iliyopo nchini.

Akizungumza na uongozi na wafanyakazi wa TIFU TV alipotembelea kituo hicho Vikokotoni mjini Zanzibar, Waziri Kombo alisema, vyombo vya habari vina nafasi kubwa kudumisha amani iwapo vitaepuka kutoa taarifa zinazofarakanisha watu.

Hata hivyo, alisema iwapo vitakengeuka maadili na miko ya tasnia ya habari, vinaweza kuwa chanzo cha kutoweka amani na usalama, akitoa mfano wa nchi za Rwanda, Burundi na baadhi ya mataifa ya Afrika Kaskazini yaliyosambaratika kutokana na kalamu za waandishi wa habari zilizotumiwa vibaya.

“Wakati wa uchaguzi bakieni kwenye kazi yenu ya kuwapasha habari wananchi kuhusiana na yanayoendelea kwa usahihi bila kutia chumvi wala kupendelea upande wowote, siasa tuachieni sisi wanasiasa,” alisisitiza.

Naye Mkurugenzi wa TIFU TV Abdalla Keisy, alimshukuru waziri huyo kwa kuvijali vyombo vya habari, akisema utendaji wake unaonesha wazi kuwa anapenda kuona tasnia ya habari inayokabiliwa na ushindani mkubwa inafika mbali.

Alisema kituo chake kipo kuwasaidia wananchi ambao sauti zao si rahisi kusikika hasa pale wanapokuwa na matatizo ya kijamii na ndio maana wakachagua kaulimbiu iitwayo ‘Kijamii zaidi’.

Alimuhakikishia waziri huyo na serikali kwamba kadiri kituo chao kinavyokua, wataendelea kufuata sheria na miongozo yote inayosimamia vyombo vya habari kwa manufaa ya sasa na baadae.

 

 

 

CHANZO: ZANZIBAR LEO

error: Content is protected !!