Skuli binafsi zatakiwa kufuata mitaala ya serikali

NA KHAMISUU ABDALLAH 

WIZARA ya Elimu na Mafunzo ya Amali, imezitaka skuli binafsi kuhakikisha zinafuata sera, kanuni, miongozo na mitaala ya wizara ili kuwajenga wanafunzi katika mwelekeo mmoja.

Mkurugenzi idara ya teknologia ya habari na mawasiliano ya wizara hiyo, Omar Said Ali, aliyasema hayo katika mahafali ya 12 ya skuli ya Lion King Junior Academy, yaliyofanyika skuli ya sekondari Haile Selassie mjini Unguja.

Alisema, kama skuli binafsi zitafuata mitaala ya wizara basi wataendana na utaratibu uliopangwa ili kuwajenga watoto katika kupata elimu bora.

Alisema kitendo cha kuwafundisha watoto mitaala ya nchi nyengine kama wanavyotumia skuli hiyo ikiwemo ya Kenya na Tanzania Bara inaweza kusababisha wanafunzi kutofanya vizuri katika mitihani yao.

Alisema serikali imefanya jitihada kubwa kuimarisha sekta ya elimu ikiwemo kujenga miundombinu imara ya elimu na mitaala.

Alisema mitaala inayotolewa na wizara ni mizuri na haipo chini ya kiwango kama inavyodaiwa na baadhi ya wawekezaji binafsi katika sekta ya elimu.

“Ili kutowachanganya wanafunzi wetu ni lazima wafuate miongozo ya Zanzibar ondoeni wasiwasi wa ubora wa mitaala yetu,” alisema.

Nae, Mkurugenzi wa skuli hiyo, Mahmoud Ibrahim, aliwapongeza wazazi na walezi kwa ushirikiano wanaotoa kwa kujenga imani ya kupeleka watoto wao kwa ajili ya kupewa elimu bora.

Akisoma risala kwa niaba ya wahitimu wenzake, mwanafunzi Huda Ahmed Issa, alisema skuli yao inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo kodi na kukosekana kwa vitabu.

Katika mahafali hayo mwanafunzi Nassir Ismail Hassan aliibuka mwanafunzi bora na kufuatiwa na  Huda Ahmed Ismail na Abdul-hakim Adam Haji.

CHANZO: ZANZIBAR LEO

error: Content is protected !!