Sunday, July 3
Shadow

Shaibu Foundation imewatunuku walimu kisiwani Pemba

WALIMU kutoka Skuli Mbali Mbali Kisiwani Pemba, wakifuatilia hafla ya kukabidhi vyeti kwa walimu waliohitimu mafunzo ya elimu mtandano na masafa, yaliyotolewa na taasisi ya Shaibu Foundation na kufanyika mjini Chake Chake.(PICHA NA ABDI SULEIMAN,PEMBA)

WALIMU nchini wameshauriwa kujiendeleza kielimu hasa katika masuala ya kimtandao, ili kwenda sambamba na teknolojia ya dunia ya sasa.

Akizungumza kwa niaba ya Afisa Mdhamini wizara ya elimu na mafunzo ya amali Pemba, Afisa elimu Wilaya Burhan Khamis Juma aliyasema hayo katika hafla ya kuwazawadia vyeti walimu waliohitimu mafunzo ya kimtandao katika Ukumbi wa American Corner Chake Chake.

Alieleza kuwa, dunia ya sasa mtandao umekua zaidi na ndio sehemu ya kimbilio la kujifunza mambo mbali mbali hususani kwa walimu wa masomo ya sayansi, civic, lugha na sayansi jamii, ili kwenda sambamba na hali halisi ya kimtandao.

“Niwapongeze walimu wenzangu kwa kuona umuhimu wa kujiendeleza ni ukweli usiofichika siku zote mwalimu hamalizi kusoma kwani kadiri tunavokwenda sasa kwenye dunia yetu ni kujifunza”, alisema.

Alifahamisha, ikiwa walimu hawatakuwa makini watajikuta wanafunzi wao ni bora kuliko wao, kwani wamekua na uwelewa mpana wa kujifunza zaidi kupitia simu zao za mikononi sambamba computer ambazo zipo katika vituo vya TEHAMA.

Aidha, aliwataka walimu hao kuyatumia mafunzo hayo kwa vitendo na kusema kuwa, mafunzo ya kimtandao endapo utayaacha yatapotea kabisa, hivyo kuna haja ya kuyatumia kwa kufundishia, ili malengo yaweze kufikiwa.

Akisoma risala katika hafla hiyo Rais wa Shaibu Foundation, Mustafa Said Moyo alisema, lengo kuu la kutoa mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo na kuwaongezea maarifa walimu wa skuli za msingi na sekondari juu ya utumiaji wa TEHAMA kama ni nyenzo mpya ya kufundishia na kujifunza.

Alisema, sababu nyengine ya kuanzishwa mafunzo hayo ni kutokana na tafiti zinazoonesha ukuwaji wa matumizi ya internet yakiongezeka kwa kasi kubwa, huku takwimu zikionesha matumizi makubwa ya mtandao huo yakitumika vibaya kama vile kuangalia picha za ngono na matumizi ya kitaaluma yakiwa chini sana.

RAIS taasisi ya Shaibu Foundation Mustafa Moyo, akisoma Risala ya sherehe ya kuwazawadia vyeti Walimu waliohitimu mafunzo ya elimu Mtandao na Masafa, kwa walimu waskuli za masingi na sekondari Pemba, mafunzo yaliyotolewa na taasisi ya Shaibu Foundation.(PICHA NA ABDI SULEIMAN, PEMBA)
AFISA elimu Wilaya ya Chake Chake Burhan Khamis Juma, akitoa nasaha kwa walumu wa skuli za msingi na Sekondari waliohitimu Mafunzo ya Elimu Mtandao na Masafa, yaliyotolwa na ya Shaibu Foundation na kufanyika mjini Chake Chake.(PICHA NA ABDI SULEIMAN,PEMBA)
MKURUGENZI wa taasisi ya Shaibu Foundation Mustafa Said Aburabi kulia akimkabidhi afisa Elimu Wilaya ya Chake Chake Burhan Khamis Juma kushoto cheti cha shukrani kwa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Pemba, wakati wa kugawa vyeti kwa walimu waliohitimu mafunzo ya Elimu Mtandao na Masafa, yaliyotolwa na ya Shaibu Foundation na kufanyika mjini Chake Chake.(PICHA NA ABDI SULEIMAN,PEMBA)

“Mradi huu ulitekelezwa kwa awamu mbili, awamu ya kwanza ulitekelezwa mwaka 2018 katika skuli ya msingi madungu ambapo walimu 17 walishiriki mafunzo na kukabidhiwa vyeti”, alisema.

Aidha alisema, awamu ya pili mradi umetekelezwa mwaka huu kwa kipindi cha miezi mitatu huku jumla ya skuli tisa zilialikwa kushiriki mafunzo na skuli tano tu ndizo zilizoonesha nia ya kushiriki.

Akitoa neno la shukurani kwa niaba ya wahitimu wenzake mwalimu wa skuli ya sekondari Makoongwe Haji Mzee Mohamed alisema, mafunzo hayo ni muhimu sana kwao kutokana na dunia ya sasa ni ya kimtandao.

Hata hivyo aliipongeza taasisi ya Shaibu Foundation kwa kuwapatia taaluma hiyo ambayo itawasaidia kufundisha kwa ufanisi zaidi.

Jumla ya wahitimu 53 wamekabidhiwa vyeti vya mafunzo ya kimtandao na taasisi ya Shaibu Foundation Kisiwani Pemba.