Polisi yatumia mabomu kuzima maandamano Uganda

Polisi yatumia mabomu kuzima maandamano Uganda

Maafisa wa polisi nchini Uganda wametumia mabomu ya kutoa machozi kuzima maandamano ya wananchi waliomiminika katika barabara za mji mkuu Kampala, kulalamikia kodi mpya wanazotozwa watumiaji wa mitandao ya kijamii.

Mbunge mmoja kwa jina Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine, na waandishi kadhaa wa habari ni miongoni mwa makumi ya watu waliotiwa mbaroni katika maandamano hayo.

Wanaharakati waliotisha maandamano hayo wamesema kuwa, kodi hiyo haijazingatia uhalisia wa maisha ya Waganda na hivyo wameitaja kuwa itakayoathiri sehemu kubwa ya raia wa nchi hiyo.

Maandamano hayo yamefanyika chini ya kaulimbiu “Kodi Hii Lazma Iondolewe”.

Mwezi Mei mwaka huu Bunge la Uganda lilipasisha sheria ya kuwatoza kodi ya Shilingi 200 (Dola 0.005) watumiaji wa mitandao ya kijamii nchini humo. Mitandao ya kijamii iliyoathiriwa na kodi hiyo mpya ni pamoja na Facebook, Twitter, WhatsApp, Google Hangouts, YouTube, Skype, na Yahoo Messenger.

Rais Yoweri Museveni anaunga mkono kodi hiyo ya mitandao ya kijamii

Kadhalika Rais Yoweri Museveni ametangaza hadharani mara kadhaa uungaji mkono wake kwa kodi hiyo, akisema kuwa mbali na Waganda kuchangia moja kwa moja katika hazina ya taifa, lakini pia itasaidia kuwabinya wanaopoteza muda mwingi katika mitandao hiyo na kueneza habari za urongo.

Hii ni katika hali ambayo, huduma za kutuma na kupokea pesa kwa njia za simu nazo zimelemazwa nchini Uganda kufuatia kupanda kwa kodi ya huduma hizo.

error: Content is protected !!