Sunday, July 3
Shadow

Dk. Hussein Ali Mwinyi amewaapisha Wajumbe wapya wa Tume ya Mipango ya Zanzibar

RAIS wa Zanzibar ambae pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akimuapisha Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Kazi Uchumi na Uwekezaji Zanzibar Mhe Mudrik Ramadhani Soraga, kuwa Mjumbe wa Tume ya Mipango,hafla hiyo iliyofanyika katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar.

 

Rais wa Zanzibar ambae pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amewaapisha Wajumbe wapya wa Tume ya Mipango ya Zanzibar.Hafla hiyo imefanyika leo Ikulu Jijini Zanzibar ikiwa ni kikao cha kwanza cha Tume hiyo katika Awamu ya Nane ya uongozi wa Rais Dk. Mwinyi ambapo Makamo wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Othman Masoud Othman na Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Hemed Suleiman Abdullah walishiriki ikiwa ni Wajumbe kutokana na vyeo vyao.

Mara baada ya kiapo hicho, Rais Dk. Mwinyi alitumia fursa hiyo kuwapongeza Wajumbe hao wapya aliowaapisha pamoja na wale wa zamani wanaoendelea.Katika pongezi hizo, Rais Dk. Mwinyi alieleza matumaini yake makubwa kwa wajumbe hao wa Tume ya Mipango ya Zanzibar katika kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Wajumbe walioapishwa ni Katibu Mkuu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Mhandisi Zena Ahmed Said, Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar Dk. Mwinyi Talib Haji,Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Fedha na Mipango Jamal Kassim Ali, Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makaazi Riziki Pembe Juma, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Kazi, Uchumi na Uwekezaji Mudrik Ramadhan Soraga.

Wengine ni Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda Omar Said Shaaban,Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Rahma Kassim Ali, Waziri wa Maji, Nishati na Madini Suleiman Masoud Makame,Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale Lela Muhamed Mussa, Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi Abdalla Hussein Kombo pamoja na Dk. Rahma Salim Mahfoudh Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango Zanzibar.

Wajumbe hao wapya walioapishwa hivi leo waliahidi kutekeleza majukumu yao kwa maslahi na uchumi wa Zanzibar.

Nao wajumbe wa zamani wa Tume hiyo ya Mipango ya Zanzibar Mohammed Faki Mohammed pamoja na Profesa Semboja Haji Hatib walitoa shukurani zao kwa Rais wa Zanzibar Dk. Hussein Mwinyi kwa kuendelea kuwaamini kuwa Wajumbe wa Tume hiyo na kuahidi kwamba wataendelea kufanya kazi kwa ajili ya maendeleo ya Zanzibar.

 

CHANZO: IKULU