Barabara nyengine yadidimia Mtambwe, wananchi wasubiri kwa saa kadhaa

Imeandikwa na Haji Nassor, Pemba:

WANANCHI wanaotumia barabara ya Wete Gando, jana wamejikuta katika mazingira magumu ya kukatisha au kuchelewa safari zao, baada ya eneo la Mangwena la barabara hiyo, kudidimia urefu wa mita saba kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha.

Tukio hilo lilitokea juzi Mei 13, ambapo wananchi waliokuwa kwenye gari wakienda mjini Wete na maeneo mengine kwa shughuli zao mbali mbali, walijikuta safari zao zikiishia hapo kwa muda, baada ya kufika na kushudia barabara ikiwa imedidimia.

Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi, walisema kufuatia hali hiyo, walilazimika kupita kando kando kwa miguu wakiwa na mizigo yao mepesi, na kisha kusubiri gari za upande mwengine ili kukamilisha safari zao.

Omar Hamad Makame, alisema yeye alikuwa anasafiri kwa ndege, ingawa kutokana na hali hiyo alilazimika kughairisha safari kwa siku hiyo, baada ya kukaa hapo kwa zaidia ya saa 3 na nusu.

“Mimi leo safri yangu ya Dar-es Salaam imeshakatika, maana muda nilioupoteza hapa kwa kusubiri mamlaka zifungue njia ya dharura sio mdogo, “alieleza.

Nae Mwanashida Yussuf Haji alisema, alikuwa anakwenda hospitali ya Wete kwa uchunguuzi wa afya yake, ingawa alilazimika kurudi kutokana na wasi wasi wake kwa safari huko mbele.

“Pengine kudidimia kule kwa barabara inawezekana na huko mbele kukajitokeza tena, hivyo bora narudi nyumbani nitakwenda hospitali siku ya pili,”alisema.

Hata hivyo baadhi ya madereva waliokataa kutaja majina yao, walisema hata baada ya wizara husika kuweka barabara ya muda, hawakujaribu kupitisha gari zao na ni vyema wakatishe safari kwa siku moja.

Alisema kutokana na ardhi kushiba maji, hata mawe na kifusi kilichowekwa kwenye barabara ya dharura kwa gari zenye uzito mkubwa ni wasi wasi kupita.

Mhandishi ujenzi wa barabaara kisiwani Pemba kutoka wizara ya ujenzi, Khamis Massoud, alisema eneo hilo la Mangwena lililodidimia ni lile lililowekwa udongo wakati wa ujenzi wabarabara hiyo ukifanyika.

Alisema sio kweli kwamba mkandarasi wa ujenzi hakuwa na utaalamu, bali ni kutokana na uwekaji wa dongo (kujazwa) na kuacha barabara ya asili ili kukimbia mipindo inaweza kuwa ndio sababu.

Hata hivyo alisema, juhudi za haraka zilianza kuchukuliwa tokea siku hiyo ya tukio, kwa kufungua barabara ya zamani na kujazwa mawe na kifusi na kwa jana gari ndogo na zenye uzito wa wastani zilianza kupita.

“Kwa kweli pamoja na juhudi zetu, ambazo tulizifanya kwenye eneo jengine, lakini kwa gari kubwa hazikuwa na uwezo wa kupita, na zilizojaribu ilibidi tuzisukume, lakini ndogo zilipita kwenye njia ya dharura,”alisema.

Katika hatua nyengine Mhandishi huyo alisema, eneo hilo lililodidimia wastani wa mita saba urefu, hawatolijenga mapaka mvua zitakapomalizika, ili wawe na utulivu ingawa udogo wake umeshachukuliwa kwa ajili ya kuchuunguzwa.

Wakati huo huo Mhandisi huyo alisema, eneo la barabara ya Bahanasa-Mtambwe kuelekea Uwondwe eneo la Kilimapunda, napo pamepasuka upande mmoja wa barabara.

Alisema eneo hilo lililipasuka upande mmoja na kwanza madereva walipata woga kupatumia, ingawa baada ya kwenda wao waliwaruhusu na panatika.

Hata hivyo ameendelewa kuwataka madereva kuwa na tahadhari katika kipindi hichi cha mvua zikiendelea kunyesha na wapohisi pahala panampasuko wasisite kutoa taarifa.

Tokea kuanza kwa mvua hizi za masika mwishoni mwa mwezi uliopita hadi Mei 13 maeneo ya barabara ambayo yameshaharibika ni Mkoani Changaweni, Mungu yuko, Kwa makanzu, Mtambwe kilimapunda na Wete Gando eneo la Mangwena.

 

 

 

CHANZO: PEMBA TODAY

error: Content is protected !!