Rais wa Zanzibar ambae pia ni  Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema kuwa Serikali itatoa tamko kuifanya siku ya mwaka mpya wa kiislamu kuwa ya mapumziko.Alhaj D. Mwinyi aliyasema hayo jana katika kongamano la maadhimisho ya mwaka mpya wa kiislamu 1444, lililofanyika msikiti wa Jamiu Zinjibar, Mazizini, Mkoa wa Mjini Magharibi.

Aidha alisema kuwa maadhimisho hayo yatafanyika kwa mzunguko kati ya Unguja na Pemba ili kutoa nafasi kwa Waislamu kushiriki.

Aliipongeza Ofisi ya Mufti Mkuu wa Zanzibar kwa kuandaa maadhimisho hayo ambayo ni utaratibu mpya kufanyika visiwani hapa na inatoa fursa kwa waislamu kujua mwaka wao kwa mujibu wa tahehe za dini yao.

“Hakuna asieujua mwaka mpya ule wa kawaida na siku ya mwaka mpya ikifika basi kila mtu anajua lakini kwa bahati mbaya sana mwaka mpya wa kiislamu watu wengi hawautambui,”alisema

Hivyo, alisema utaratibu wa kuadhimisha mwaka mpya wa kiislamu utawakumbusha Waislamu kuujua.

Aidha, Alhaj Dk. Mwinyi aliwakumbusha wananchi kushiriki zoezi la sensa ya watu na makazi Agosti 23 mwaka huu kwa sababu lina umuhimu katika kupanga maendeleo ya nchi.

Nae Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora, Haroun Ali Suleiman,  alimuomba Dk.Mwinyi kuifanya siku ya mwaka mpya wa kiislamu kuwa ya mapumziko ili waumini wa dini hiyo wapate fursa ya kusherehekea siku hiyo na familia zao kama zilivyo siku kuu nyengine.

Mapema Mratibu Mkuu wa Kongamano hilo, Sheikh Khalid Ali Mfaume, alisema lengo la maadhimisho hayo ni kuwakumbusha waislamu wajibu wao wa kujua tarehe za uislamu.

Alisema sheria nambari 4 ya Ofisi ya Mufti Mkuu wa Zanzibar ndio iliyowezesha kufanyika kongamano hilo pamoja na shughuli nyengine zilizoandaliwa.

Akitoa mada kuhusu sensa na uislamu, Sheikh Khamis Abdulhamid, alisema sensa imetajwa ndani ya Quran na uislamu haukatazi watu kuhesabiwa kwani ni muhimu kwa sababu inasaidia kupanga maendeleo ya baadae.

Alisema, sensa maana yake ni kujua idadi ya watu na makazi yao na namna walivyo katika maendeleo ya kiuchumi.

Kongamano hilo pia lilihudhuriwa na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Massoud Othman, Makamu wa Pili wa Rais, Hemed Suleiman Abdalla na viongozi wengine wa vyama na serikali.